Miaka Kumi Baadaye, Nakukumbuka Babangu!

Standard

Tarehe kamili kama leo miaka kumi iliyopita, jambo lililobadili maisha yangu kabisa lilitokea. Asubuhi Desemba tarehe 2 2001, nilijinyanyua kwenda kufunga mfereji wa maji uliyokuwa ukichuruzika usiku kucha. Baba alikuwa amenikumbusha kuufunga vyema kabla kulala ili maji yatakapofunguliwa usiku katika bomba kuu la jengo letu, yasipate kumwagika. Ni agizo ambalo nilisahau kutimiza na hivyo kulazimika kuamka alfajiri na mapema saa kumi na moja kwenda kuzima. Kibaridi kisicho cha kawaida kilinipiga mwilini na kunifanya kuganda. Nilihisi kuwa kuna jambo lisilo la kawaida linalonitendekea lakini sikujua ni wapi au vipi.

Nilihofia manake nilidhani nitampata baba ameamka kama ilivyokuwa desturi yake ili ajitayarishe kwenda kazini. Laiti ningalijuwa yaliyonisubiri! Nikakwenda mlangoni mwa chumba alimolala baba na kubisha mlango kwa upole. Baba! Baba! Baba! Niliitana lakini sikupata jawabu. Jambo ambalo halikuwa la kawaida.

Kwa utaratibu mkubwa niiliiufungua mlango na kuingia. Nikanyatia kitandani alikolala baba na kuanza kumtikisa huku nikimwita. Niliona kuwa alikuwa amechelewa kuamka ili kujitayarisha kuenda kazini na iwapo angeendelea kulala hivyo basi angechelewa kufika kazini.

“Baba! Amka baba wakati umefika” masikini niliitana nisipate jibu. Jambo lililonipa msukumo wa kumfunua. Lo! Baba alikuwa amelala kwa utulivu na kuunyosha mwili wake kabisa. Alikuwa kasha lala usingizi usiojuwa wakati wake wa kuamka. Kama mchezo tena kwa ghafla, babangu mzazi alikuwa ameaga katika usingizi wake. Niliona dunia yangu ikizunguka na macho karibu yanitoke maanake sikujua pa kuanzia. Asubuhi na mapema vile, na umri wangu mdogo wa miaka kumi na mitatu  tena katika darasa la saba, ningeanzia wapi ilhali familia yetu ilikuwa katika mji tofauti na mimi ndiye niliishi na baba? Ilikuwa mwaka wa 2001. Yaliyofuatia yalibaki kitendawili kwani sikuwahi amini ya kuwa baba yangu alikuwa ameaga hadi mwaka wa 2005!

Sasa napiga darubini yangu nyuma, mengi yamejiri mno katika familia yetu ambayo sina budi kumshukuru Maulana kwa majaliwa yake. Ndiye Mungu mwenye kutujalia neema ndogondogo na neema kubwa kubwa. Babangu akifufuka leo, atashtuka kumpata mwanawe wa kwanza alijitaidi masomoni hadi kukamilisha chuo kikuu na kwa sasa ninachapa kazi! Ajabu maanake aliniwacha katika darasa la saba wakati hata masomo ya msingi sikuwa nimemaliza.  Wenzangu wanaonifuata pia wamejitahidi na kuingia katika vyuo vikuu na wengine kukamilisha masomo ya sekondari.

Zaidi ya  yote, daima namshukuru mamangu mzazi. Amekuwa kipa imara kwetu katika miaka hizi zote na kutia bidii kama za mchwa kuwapa wanawe maisha bora. Isingalikuwa mamangu, nisingelikuwa nilipo. Amekuwa mnara wetu nyakati zote! Alinipa tabasamu na sababu ya kuona siku mpya hata nilipodhani kuwa yote yamekwisha.

Advertisements

MAUTI YALIBISHA MLANGONI

Standard

Daktari Mogiri alifungua mlango polepole na kutoka nje. Alinikuta nimeketi kwa fomu ndefu hapo nje ya wodi nikisubiri. Nilikuwa nimejishika tama na kuzama katika luja ya mawazo. Ni kweli kwamba mshika tama huwa analo moyoni.nilimwangalia kwa macho ya atiati nikitazamiakusikia mengi kumhusu mke wangu Zuhura. Sikujua kilichomtendekea tangu aingizwe mle ndani ya chumba cha upasuaji, masaa matano yaliyopita. Kumbe kweli usilolijua ni kama usiku wa manane.

Akilini mwangu, yaliyotendeka yalikuwa yangali mbichi mno. Nilitoka kazini mapema alasiri hiyo na kurudi nyumbani kwani sikuwa na kazi nyingi ya kufanya. Nikafululiza hadi mlangoni na kubisha bila kupata jibu.wanenao husema kuwa kimya kingi kina mshindo. Nilifungua mlango polepole na kuingia ili kugundua kilichonisubiri. Lo! Ukistaajabu ya musa utayaona ya firauni.

Zuhura alikuwa kalala sakafuni, akigaaga na kufurukuta kwa uchungu na kutoa sauti ya maumivu. Aliye na macho haambiwi tazama. Nilielewa fika kuwasiku zake za kujifungua zilikuwa zimewadia. Kasha akajikazana kutamka,

“Nisaidie jamani.” Kisha akanyamaa ghafla na kuendelea kufurukuta. Fimbo ya mbali haiui nyoki kwa hivyo, niliwaita majirani walionipa usaidizi wa kutafuta rukwama ili kumpeleka hospitalini. Ilikuwa nadra na adimu kama wali wa daku kuona magari katika sehemu tuliyoishi. Sehemu ya Ngomani. Kama wakaazi wa pale, tulizoea maisha hayo na haikuwa ajabu kumwona akipanda au kuabiri ‘gari’ letu- rukwama. tulimpeleka kwa zahanati ya kipekee hapo mjini na kupata kuwa muuguzi hakuwepo. Nikawa nimechanganyikiwa nisijue la kufanya  jirani mmoja aliposhauri tumkimbize Zuhura katika hospitali ya wilaya.

Hospitali ya Afueni ilijulikana kote kwa kuwa ya bei ghali. Lakini nilishawishika na kukubali kwani maisha ya Zuhura ilikuwa muhimu kuliko pesa. Tukaandamana hadi kule. Hisia za uchovu na kutamauka tayari zilianza kuninyemelea nikawa nafuata wenzangu tu kama bendera inavyofuata upepo au maji inavyofuata mkondo. Moyo wangu ulijaa ukunjufu kwa ukarimu walionionyesha.

Nikawa nimeketi hapo nikisubiri matokeo ya daktari waliokuwa wakimhudumia. Takribani miaka mine sasa tangu tufunge ndoa, Zuhura alibaki tasa asiweze kupata motto hata mmoja. Mara nyingi nilimsikia akimlilia Muumba wake na kusali. Hatimaye maombi yake yalijibiwa na sasa tulikuwa tukitarajia mwana wetu wa kwanza. Tayari nilikuwa na cheche za matumaini. Penye nia pana njia eti. Hata nikakisia kuwa atakuwa msichana na tungemwita Zawadi. Pengine kama ishara kuwa Maulana alitupa zawadi baada ya miaka. Nilisahau kabisa onyo la wahenga eti usikate kanzu kabla motto hajazaliwa.

Daktari Mogiri akanisongelea na tukaanza majadiliano. Mazungumzo ya kiume kama alivyoyataja. Mara kwa mara niliwaona wauguzi wakipitapita kushoto-kulia wakiendelea na shughuli zao. Daktari alikuwa amemaliza kazi yake muhimu mle ndani.

“Unatarajia mtoto wa jinsia ipi? Mbona? Mtamwita nani? Utampa Zuhura zawadi gain kwa kazi aliyofanya?” aliniuliza maswali chungu nzima. Maswali yenyewe yakatuongoza katika ulimwengu wa gumzo. Tukazungumza na kupitiza wakati bila hata kugundua. Hata chembechembe za wasiwasi nilizokuwa nazo zikanitoka kabisa. Nikajihisi huru, kiumbe mpya na nikavaa piku la tabasamu.

Ndipo sasa daktari akaamua kunipasulia mbarika hatimaye. Akanidokezea kuwa  Zuhura alikuwa amejifungua motto wa kiume mwenye buheri wa afya. Singejizuia tena.licha ya kuwa usiku ulikuwa umeingia, nilirukaruka kwa furaha kupindukia ungedhani mwenda wazimu. Nikatamani majirani wote waliomleta Zuhura wangalikuwepo lakini walikuwa washarudi makwao kushughulikia jamii zao.       Nikaanza kuwazia jina la motto wetu nikiwa katika hali ya kurukaruka bado.                                           “Tutamwita Bahati” Nilisema kwa nguvu huku nimemkumbatia daktari kwa furaha macho yangu nikiwa nimeyafumba.

Daktari alikuwa akinitazama tu kwa wakati wote huo pasi na la kusema. Lakini nilipoanza kuuelekea mlango wa chumba alimolazwa mke wangu, alinisitisha na kunizuia. Akaniomba kusubiri lakini furaha iliyonijaa ikanifanya kuwa kiziwi. Nikajitia pamba masikioni nisisikie la mwadhini wala la mteka maji msikitini.

Akanivuta kando kidogo na kunidokezea kuwa Zuhura mwenyewe alifuja na kupoteza damu nyingi hivyo basi asingeweza kuishi! Kwa kifupi, aliniambia kuwa mke wangu alikuwa amea…sikuyaamini macho na masikio yangu. Maneno hayo yalinifanya kiuwa chakaramu zaidi. Yalinikata maini, yakanikera na kunikereketa ajabu. Uso wangu uliokuwa na furaha ulibadilika ghafla na kufinga. Kwa nguvu kama za tembo na hasira za mkizi, niliuendea ule mlango bila kumjali yeyote wala chochote. Alinifuata na kujaribu kunivuta nyuma huku akiniliwaza. Juhudi zake zikangonga mwamba.

Sikujua kuwa daktari ni watu wenye vipawa vha kuwapumbaza watu namna hiyo! Kwa muda wote huo, daktari alikuwa amejua ukweli na kunificha kwa kunishirikisha katika mazungumzo. Pengine hayo ni baadhi ya mafunzo wanayopewa wanaposomea fani ya udaktari lakini ubunifu wa ya Mogiri ulishinda wote. Niliajabia ubunifu wake!

Niliingia kwa fujo na rabsha kama mfungwa aliyeachiliwa huru. Wauguzi wakashtuka na kujaribu kunizuia. Daktari akaingia na kuagiza nionyeshwe mtoto. Nikaelekezwa hadi alikokuwa. Mtanashati ajabu na mwenye afya ungedhani kutoka mbinguni. Alilala kwa utulivu asijue mamake alikokuwa. Laiti angejua. Lakini kuonyeshwa mtoto haikunisaidia wala kinutuliza. Nani angekilisha,akivishe na kukilinda siku zote? Unyama upi huo kuingizwa katika ulimwengu na kuachwa na mwenyeji wako hata kabla ya kumwona ana kwa ana? Nilijihurumia, nikamhurumia malaika wa Mungu. Machozi yakanidondoka kama mtoto na nikayaacha kumwagika bila aibu.

Kwa mwongozo wa daktari, nilifululiza hadi alikolazwa Zuhura. Msichana mrembo aliyeumbwa akaumbika alikuwa amelala kwa upole na utulivu asijue hata wakati wa kuamka. Alikuwa amefunikwa vizuri hata usingedhani ni maiti. Ikanifanya kutoamini na kuanza kumwamsha. “Zuhura, amka umwone Bahati mwana wetu.”

Akawa haoni, hasemezi,hatikisiki. Kimya kikajiri. Niliinama  kando yake na kumtikisa tena mara hii kwa nguvu machozi zaidi yakinitoka. Nikamshauri ainuke twende kwetu tusherehekee kuzaliwa kwa mtoto wetu. “Zuhura” niliita mara ya mwisho kwa nguvu na pumzi ikaniishia.

Sauti nyororo ya Zuhura aliyekuwa amelala kando yangu usiku wote ilinigutusha kutoka usingizini ikinijuza kuwa kumekucha. Miale ya jua nayo ilikuwa imeshachomoza nje. Furaha iliyoje kupata kuwa hiyo ilikuwa ndoto ya ajabu.

UVUVI ZIWANI

Standard

Jua lilikwisha zama lakini bado nyuma liliacha mikia yake ya uchengu wa mwangaza uliopinganisha rangi tofautitofauti kama ishara ya heri njema kwa wote walioipenda siku hiyo.Hadi kufikia wakati huo, bado tulikuwa baharini tukikamilisha shughuli zetu za uvuvi. Kweli ilikuwa siku njema. Tulibahatika kuwavua samaki wengi mno. Pengine kwa sababu unyavu wetu ulikuwa ungali mpya. Tulifurahia na kuchangamkia jambo hili hata tukawa tunapiga soga kwa ucheshi mwingi tukiisukuma mashua yetu kufelekea ukingoni mwa ziwa kwani kilicho na mwanzo kina mwisho.

Mara kwa ghafla bin vuu, upepo mkali ukaanza kuvuma kwa nguvu kama za tembo. Mawimbi yakawa yameanza kujitunga tayari ziwani. Yalionekana yakijibeba, yakijiinua na kujibwaga tena kwa nguvu. Mawingu mazito tena meusi ti yakuogofya na kutisha yalikuwa yamekusanyika angani. Dalili ya mvua ni mawingu.

Kuona vile,sote tuliingiwa na wasiwasi kama wa kuku mgeni. Mambo yalikuwa yakitambarika kila muda ulipozidi kuyoyoma. Ndiyo sasa tulikuwa tumefika katikati ya ziwahilo. Kwa utaratibu, mashua yetu ilianza kuongeza uzito hadi ikawa nzito kama nanga.isitoshe, Samaki tuliokuwa tumewavua pia walichangia uzito kuongezeka.

Liloogofya zaidi ni kuwa hapakuwa na wavuvi wengine ziwani. Wote walikuwa washatoweka, wakatokomea na kuvogomea katika peo za macho yetu. Walikuwa wamerudi viamboni mwao kujiunga na jamaa zao. Nyoyo zetu zilitututa kwa nguvu kwa hofu. Upepo mkali ukaanza na kwa umbali tuliona miti zikiinama kusalimu amri. Lililonijia akilini ni tukio lililomkumba Yesu na wafuasi wake kama nilivyopata kuona kwenye sinema awali. Yesu alionekana kuunyosha mkono wake na kuamuru mawimbi kutulia na ghafla yakapoa. Nami bila kusita niliunyosha mkono wangu kama Yesu na kuyaamuru kutulia, jambo lililowafanya Nguviu na Suluhu kuangua vicheko licha ya hali iliyotawala. Lakini hakuna kilichobadilika. Pengine hatukuwa na imani dhabiti katika Bwana.

Badala yake, mashua yetu ikaanza kuingia na kuzama majini. Tulijaribu kupunguza kiimo cha mashua yetu kama hatua ya kwanza. Ungeona namna walivyoruka, kuogelea na kupotelea majini kwa furaha, ungedhani ni wafungwa wameachiliwa huru baada ya hukumu ya kifo. Uzani ukapungua kidogo na tukarejelewa na cheche za matumaini.sote watatu tukawa tunasukuma mashua yetu kwa furaha. Tukaamua kufanya chapuchapu kuiondoa mashua yetu humo ziwani kwani giza lilikuw limeanza kutawazwa angani. Tena tulitaka kuondoka kabla mvua kuanza kunyesha. Wahenga huonya eti tahadhari kabla ya hatari.

Sikuona wala kujua namna Suluhu alivyorudisha unyavu majini. Alitugutusha alipoanza kucheka na kuitana tumpe usaidizi wa kuuvuta unyavu huo kwani ulikuwa na windo nono. Nani asingefurahi? Tena umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu na aidha kidole kimoja hakivunji chawa. Sote tukauangana na kuanza kuburura hadi hapakuwa na dalili zozote za wavu kusonga.

Sululu alisonga mbele zaidi na kuburura kwa nguvu zake zote na lo! Samaki mkubwa alijitokeza kwa rabsha,fujo, vurumai na kishindo na kisha kuzama ghafla na kufanya mashua yetu kutingizika. Kumbe mkia wake ulikuwa katika sehemu ya chini ya mashua yetu ndani ya maji. Hili tuligundua kwa namna mashua yetu ilivyorushwa. Tukawa majini tukipigania maisha yetu. Kwa mara ya kwanza nikakutana na kifo ana kwa ana. Tulianza kupiga mayowe kutaka usaidizi lakini vilio vyetu viliambulia patupu.

Ikawa kila mtu na mzigo wake kwani mvua kubwa ilikuwa ishaanza kunyesha. Ngurumo za radi zilisikika na nguo zetu zikaloa chepechepe. Tukawa sasa ni kuogelea, haswa mimi niliyesalia na wiki moja tu kukalia mtihani wangu wa kitaifa wa kidato cha nne. Mashua yetu ilisombwa na maji na kuenda mbali mno. Potelea pote! Heri uzima kuliko mashua. Tulikuwa tumeogelea na hata kukaribia sana ukingoni.

Lakini kila mara maji yalituzidi nguvu. Kumbe tulijiingiza katika ziwa bila mbinu toisha za kuogelea. Susulu alichelewa kupiga mayowe kwani tulipomsikia akifanya hivyo, tayari alikuwa akisukumwa na maji. Alikazana kutufikia na kutupa mkono wake lakini nguvu zilionekana kumwisha hadi akwa anapelekwa tu kama gogo. Tulijaribu kadri ya uwezo wetu kumfuata lakini wapi! Alikuwa keshakwenda zake. Msomaji, hisia zetu baada ya hapo zilikuwa hazielezeki.

Tulipokuwa mita chache tu karibu na ukingo wa ziwa, Nguviu naye alilalama eti mguu wake ulikuwa umekamatwa na kitu kisichojulikana. Nikainua kichwa zaidi juu ya maji na kutamka kwa shida nikimwarifu kujikaza kufika ukingoni ili suluhisho lipatikane. Huo haukuwa wakati wa kusema mengi kwani maji yaliingia kinywani. Lakini aliendela kunung’unika zaidi.

Nilionekana kujua kuogelea zaidi. Nikamwambia aushikilie mguu wangu mmoja nami niogelee hadi mwisho kisha nimvute. Japo ilikuwa ngumu kuogelea katika hali hiyo, nilijaribu na kufika ukingoni salama. ‘Mungu hamwachi mja wake.’ Nilisema kwa sauti. Mimi ndiye nilitangulia na kuona kipande cha gogo. Nikafurahi na tabasamu hafifu ikaonekana usoni mwangu.

Bila kukawia, nililipanda gogo lenyewe na nikawa sasa namshawishi Nguviu kuunyosha mkono wake niukamate, kasha nimvute pia. Cheche za matumaini zilizotoweka awali zikarejea tena. Nguviu aliukaribia mkono wangu kwa utaratibu. Akaunyosha wake, nikaukamata na kuanza kumvuta.

Mara tu aliponipa mkono wake wa pili, alivutwa ghafla na mara hii akazama zii. Nilikuwa tu nimeanza kupiga mayowe wakati lile gogo nililopanda lilizama pia na kunitumbukiza majini. Kumbe alikuwa ni mamba niliyemkanyaga kwa wakati huo wote! Kila kitu kikawa giza totoro kwangu.Nilipiga usiahi mkali na kujaribu kufungua macho. Ndipo nikagutuka kutoka usingizini. Nilikuta darasa zima linanizomea huku Susulu na Nguviu wakifa kwa vicheko vilivyopenya angani kana kwamba walikuwa na fununu ya kile nilichoota. Nduru ndiyo ilimfanya mwalimu wa Bayolojia kugundua kuwa nilikuwa nikilala darasani wakati wote tangu alipoanza kufunza alasiri hiyo. Nilijua kilichonisubiri  baada ya kipindi kukamilika.

MDUDU ALINIUMA

Standard

Mbinguni, jua lilikuwa limemaliza kazi yake na sasa lilijikokota magharibi huku mionzi yake miekundu ikiwapungia walimwengu kwa ulegevu kana kwamba kuwashukuru wale wote walioipenda. Masikini nilibaki pale uani nimelitumbulia macho, huku machozi yakijikusanya tayari kumwagika. Heri ningekuwa jua. Nisingekuwa na wasiwasi wa swala lolote. Langu lingekuwa tu kuchomoza asubuhi na kutua jioni.

Nilikuwa nimechoka kuwatazama wapita njia na magari ya kifahari. Yalikuwa mapya na yalikwenda kwa kasi tena bila kutoa sauti. Lakini kuna yale yaliyochakaa yenye breki zilizokwaruzana kila yaliposimama. Watu nao walipita wa aina tofautitofauti; si weusi, si weupe, warefu kwa wafupi na hata vijana kwa wazee. Kwa umbali,taa za umeme zilikuwa zimelimwaia jiji mchana bandia wa mwangaza. Ishara kuwa usiku ulikuwa unaingia na giza kuanza kutawazwa.

Yote hayo sikuyaonea fahari tena. Mambo yalikuwa kangaja kumbe na sasa yalikuja. Niliketi nikiwazia matokeo ya daktari, ambayo niliyapokea takribani miezi miwili iliyopita. Awali, walinificha ukweli lakini niliposisitiza, nilipasuliwa mbarika. Laiti wasingelinijuza kwani tangu hapo maisha yangu yalichukua mkondo tofauti mno. Mwenyewe, ile hamu na tama ya kula vyakula iliniondokea. Nikawa sili lolote, sinywi chochote. Mashavu yangu yalizidi kushobwekea ajabu. Nguo zangu ningezivua, mbavu zingehesabika hadharani moja baada ya nyingine. Nyele zangu zilizokuwa ndefu na nyeusi ti sasa zilibadili rangi na kuanza kuchipuka ovyoovyo. Mdudu alikuwa ameniuma. Lakini yupi?

Darubini yangu ilinikumbusha mambo yalivyoanza. Yote yaling’oa nanga baada ya kumaliza kidato cha nne. ‘Mrembo’ nilijidai kwenda jijini kutafuta kazi ya ukarani. Niliwahakikishia wazazi kuwa nilikuwa na rafiki wengi waliojitolea kunipa makao wakati nikitafuta kazi. Wavyele wakadinda kuniruhusu mwanzoni lakini baada ya kuzidi kusisitiza na kufanya kiburi nyumbani, waliafikiana na kuniacha kwenda zangu. Pengine walikumbuka kuwa mtoto akililia wembe mpe. Nilipokuwa nikiondoka, mama alikuwa na huzuni mno na kwa uchungu, alinionya kuwa mwenda tezi na omo marejeo ni ngamani. Potelea pote. Sikutaka kusikia ya yeyote kwani nilijitia hamnazo nisikie la mwadhini wala la mteka maji msikitini. Nikawa binti kiziwi asiyesikia anayoambiwa.

Kazi baada ya kuikosa,nilijiunga na wenzangu na tukajiajiri wenyewe. Malipo yakawa ya kuvutia ajabu kwani wateja walivyoongezeka ndivyo malipo yalivyoongezeka. Alimradi ujue namna ya kuwaongelesha na kuwahudumia wateja sawasawa. Jambo ambalo nilijifunza kufanya hata nikabobea na kutopea katika nyanja hiyo. Waume niliwabadili kama nilivyobadili mavazi yangu kwa siku. Nikawa ndiye jogoo la shamba lililowika jijini. Nikazika katika kaburi la sahau kuwa jijini kuna papa na papaupanga, ambao ukiwapapia, hukosi kupapatika kwa majuto, dhiki na mateso kama hayo yaliyonikumba sasa. Lau kumbe mwiba wa kujidunga hauna kilio.

Kutoka hapo uani nilikoketi, taa za umeme nilizoziona zilinikumbusha mengi. Kuhusu mienendo yangu ya awali nilipokuwa kipusa ajabu. Niliingia kwa vilabu hivyo vyote vya usiku huku mikono ya watu tofauti yamezinga kiuno changu chembamba kama cha nyigu. Daima kucha zangu zilizokuwa ndefu na zilinaksishwa rangi sawia na nguo zilizovalika.  Mdomo wangu ukakolezwa rangi nyekundu kana kwamba nililamba damu mbichi. Lakini kumbe dunia mti makavu kiumbe usiuegemee.

Watu hao niliowatazama waliniongezea uchungu mtupu. Moyo wangu mchanga ulijaa uchukivu na furaha ikawa imeyeyuka kama kipande barafu katika utupu wa mchanga wa jangwa la Sahara. Wale wasichana warembo waliovalia mavazi yaliyoacha sehemu za miiliyao kuonekana waliniudhi zaidi. Laiti wangelijua kuwa dunia itawararua na kuwaacha uchiuchi, wasingefika hata barabarani. Nilitamani kuwafikia niwaonye na kuwapa ukweli wa mambo kuhusu madhara ambayo yangewasibu lakini nilishindwa. Mimi pia nilikuwa hivyo na sasa nilikuwa naangamia. Nikakumbuka kuwa asiyefunzwa na mamake hufunzwa na ulimwengu.

Waume nao niliwatazama kama wanyama mwitu waliovalia suruali ndefu na sharti tofauti. Wanyama wenye uwezo mkali wa kukuvamia wakakumaliza kabisa. Wao ndio walionipa maji machafu yaliyokuwa na mdudu ambaye aliniuma na kunifanya kuugua sasa. Niliwatazama kwa uchukivu mwingi.

Raha nyingi ya ulimwengu ulitoweka na badala yake ikawa sasa ni huzuni tupu na majuto. Sasa niliishi kwa jumba hilo kubwa peke yangu. Ulimwengu ulinitenga kana kwamba mwenye ukoma. Wale wote waliokuwa wakiingia na kutoka siku nzima hata usingewaona. Dada yangu mdogo ndiye alijitolea kuniuguza pale kwani sikutaka kuishi na wazazi na kuwapa mzigo wa kunitunza. Ikanijia kuwa mla nawe hafi nawe ila mzaliwa nawe. Sikujua wa kumlaumu. Wazazi? La wao walinitakia mema na kunionya kusoma kwa bidii. Marafiki? Kwa kiasi kidogo lakini ndimi niliyekubali kudanganywa. Ulimwengu? Ndiyo lakini sehemu gani ya ulimwengu? Mimi ndiye wakulaumu na sasa mwiba wa kujidunga hauna kilio.

Ndoto zangu zote zilitoeka kama ukungu na umande. Azimio langu la kutaka kuendeleza masomo katika chuo kikuu katika fani ya sheria, na kufuzu katika uzamifu na uzamili lilitoweka ghafla kama mwangaza wa mshumaa uliozimwa na upepo. Nilitoka uani na kuingia katika chumba changu cha kulala. Mezani, kulikuwa picha yangu ya awali.nilijiangalia tena na kujiona tofauti; mnene, mwenye sura ya maji ya kunde tena mcheshi ajabu. Lakini sasa nilikuwa kama shetani hata ingawa sijawahi kuonana naye ana kwa ana. Haina maana kuishi katika hali hiyo! Niliifikia kalamu na kuandika kitu kwa karatasi iliyokuwa hapo kando. Kasha nikavuta kijichupa kilichokuwa hapo juu na kupiga makopo kadhaa ya yaliyokuwemo. Maini ya kaanza kukeketeka na koo kuungua ndanindani. Heri nife niiondokee dunia. Safari yangu ya kuenda jongomeoni ikawa imeanza nilikolala sakafuni.

Niligutuka usingizini nikihema na kutweta kwa nguvu mno hata nikashindwa kuendelea kulala. Ilikuwa ndoto ya ajabu.

UTENGANO

Standard

“Mimi sitakubali hilo lifanyike hata kidogo humu nyumbani. Heri nimwondokee kuliko kuwa na mke mwenza.” Nilisikia sauti ya mama ikija juu. Baba naye aliguruma kwa sauti akimwarifu mama kuwa ni wajibu wake kumrithi huyo mjane na kuwa hakuna kitakachomzuia. Majibizano hayo makali baina yao yalinifanya kuingiwa na wasiwasi. Nilikuwa sebuleni nikifanya marudio ya mwishomwisho kwa matayarisho ya mtihani wa kitaifa. Runinga nayo ilionyesha pasi na wa kuitazama.

Nikasikia tena sauti ya mama ikija juu, mara hii akitaka kupewa talaka na baba. Sauti yenyewe ilinifanya kunyanyuka halahala kutoka nilikoketi. Nikapitia mlango wa kati na kuelekea ndani kulikokuwa chumba chao cha kulala. Nikaegeza sikio langu mlangoni ili kusikia vyema yaliyokuwa yakisemwa. Nilijua vizuri kuwa huo ulikuwautovu wa nidhamu lakini nililazimika kufanya hivyo kwani pasipobudi hubidi.

Sauti ya baba ilisikika ikimwonya mama kuufyata mdomo wake au aongezwe nyingine. Nikawa bado nawazia lile baba alidhamiria kumwongeza mama niliposikia mlipuko wa ghafla, uliofuatiwa na usiahi mkali wa mama. Kishindo kikubwa kikasikika sakafuni pu! Sasa nilikuwa nimepata fununu kuhusu yaliyokuwa yakiendelea baina yao wawili tangu Muge, nduguye baba kuipa dunia mkono wa buriani mwezi mmoja uliopita.

Nilisikia kwato za baba zikiukaribia mlango na harakaharaka nikarejea sebuleni na kuketi kwenye zulia sakafuni, mara hii karibu na runinga. Sio kwamba nilitazama  filamu iliyokuwa ikiendelea bali nilikuwa nikiwazia yaliyokuwa yanatusibu usiku huo. Vita vilikuwa baina ya baba na mama lakini kama motto wao wa pekee, niliathirika pakubwa. Kweli mtego wa panya huingia waliomo na wasiokuwemo.

Kwa nguvu, nilisikia miguu ikitembea kwenye ushoroba na kukaribia sebuleni. Mlango ukafunguka ghafla na baba akaingia nilikokuwa. Kwa mitazamo ya kuibia, niligundua kuwa macho yake yalikuwa mekundu ajabu. Uso wake ulifinga na tabasamu huioni tena.nilimtazama kwa uchukivu mwingi. Nilinyamaa kama maji kwa mtungi kwani nami ningepata kichapo cha mbwa usiku huo kwani ukiona cha mwenzako chanyolewa chako tia maji.

Nilisimama kwa utaratibu na kuelekea mle chumbani alimokuwa mama. Nilikuwa nimeukaribia mlango tayari kuufungua sauti ya baba iliponguruma kunionya utoingia mle.mnyonge hana hiari. Nilitii maagizo shingo upande. Nikatamani kumjibu lakini nikameza mrututu kwani samba akinguruma mcheza ni nani? Kwa muda mrefu kimya kilijiri na kutawala baina yetu, isipokuwa mtima wangu uliosikika ukipabapaba kwa nguvu kama mtambo wa jenereta. Kimya kingi kina mshindo. Baba aliyakodoa macho yake kwenye runinga na kujitia hamnazoasjue kilichokuwa kikiendelea. nilitamani kubonyeza kitufe kilichokuwa mbele yangu ili kuizima lakini nikabaini yale ambayo yangenisibu usiku huo.

Mlango ukafunguka na mama akaingia sebuleni. Nikatambua kuwa shavu lake lilikuwa limevimba ana macho kufura kama ishara ya dhiki aliyopata hata ingawa alijifanya mcheshi.nilimfuata kuelekea jikoni. Ghafla baba akaingia mle akitaka chakula cha jioni.

“Kamwendee huyo Amira aje akupe…” hata kabla kukamilisha sentensi yake, baba alimfikia na kuanza kumzaba makofi. Mara hii, mama hakulimatia. Vita vikawa vimeanza tena, mara hii wapiganaji wakielekea sebuleni. Mama alipata msukumo uliomfanya kunifikia na hata sahani niliyobeba ilinitoka mkononi na tang! Kuanguka sakafuni ikapasuka vijipande. Nilijiingiza kati yao na kujaribu kuwatenganisha huku machozi yakinidondoka pia. Uchungu wa mwana kuwaona wavyele wake wakivurugana ukaniingia na kunidhurubu kwelikweli. Kwa kiasi kidogo, kuwepo kwangu kati yao iliwazuia kupigana. Baba alikuwa ameumwa shavuni na miwani yake kupasuliwa. Akawa anazungumzia kumdunga mama kisu afe. Akamsukuma mama kwa nguvu na kumfanya kuanguka kwa kishindo akanjigonga ukutani na mapua kuanza kuvujaa. Baba naye akajibwaga kochini akihema na kutweta kama aliyetoka mbioni.

Machozi yalizidi kunitiririka na nikatamanikuwaita majirani lakini mlango ulikuwa umefunwa ndi! Na baba. Nilitazama saa ukutani. Akrabu ziliashiria saa nne unusu. Kumbemavutano hayo yalikuwa yameendelea kwa masaa mawili mtawalia. Kando yake niliona picha ya wazazi wakifunga akidi za maisha. Picha yenyewe ilimwashiria baba akimvisha mama pete. Mama naye alijaa tabasamu usoni na kuonekana mrembo kupindukia. Kasisi pia alionekana akishuhudia na waumini wakishangilia. Kumbe kweli mambo ni kangaja.

Kilichounganishwa na Mungu kanisani mbele ya hadhira, sasa kilikuwa kikitenganishwa kisiri na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Sababu ya swala nyeti la urithi wa mke, jambo ambalo nililiona kama tamaduni iliyopitwa na wakati. Nilijilaza sakafuni angalau kusali iwapo sala ingesaidia kuokoa jahazi lililokuwa likizama. Daktari mzima kama mama ambaye huwatibu wagonjwa sasa alikuwa akigaaga sakafuni kwa maumivu pasi na wa mbinu zozote zakujisaidia. Kumbe kweli mganga hajigangi. Nilimhurumia mama na kumchukia babangu. Kwa mara ya kwanza nikatamani kuwa muuguzi, nimpe mama usaidizi na huduma ya kwanza.

Baba naye, mwanasheria muungwana alikuwa amevunja sheria kwa kuendeleza taasubi za kiume nyumbani na kumpiga mama. Ni kweli kwamba mvunja nchi ni mwananchi. Nikaapa kutoshiriki katika ndoa iwapo hayo ndio mazao ya mapenzi na ndoa. Tena nikatamani kuwa hakimu ili nimpe baba hukumu ya kumfa maishani na kumfunza adabu. Nikashindwa la kufanya na nikajilaza sakafuni huku macho yamevimba na kichwa kuniwanga kutokana na kulia kwa muda mrefu.

Akanifikia mama na kuushika mkono wangu wa kulia na kuninyanyua.

“Amka twende zetu. Mahala hapa si salama kwako mwanangu.” Alisema mama huku akinifuta machozi. Akaonyesha bayana kuwa uchungu wa mwana aujuao ni mama. Kusikia hayo, baba pia aliinuka na kunifikia. Akaushika mkono wangu wa kulia.

“Popote huendi mwanangu kwani nyumbani ni nyumbani hata kama hapakaliki.” Alisema na kunipa busu hata penzi la baba kwa mwana likadhihirika waziwazi.

Wote hawa niliwapenda sana. Ningemfuata nani? Mtihani wangu ningeufanyia wapi na tamaduni zilizopitwa na wakati madhara yake gani? Maswali yalinihujumu mno. Wote walikuwa wakinivuta upande wao. Walikumbuka usemi wa wahenga kuwa kila mwamba ngoma huvutia kwake. Nilimtazama mama. Nikamwangalia baba. ‘Fanya uamuzi wa haraka.’ Nilijiambia kwani sasa familia yetu ilikuwa inatengana milele.

MWANZO MWEMA SIO MWISHO MWEMA

Standard

Midundo ya kiafrika

Magoma bi bi bi! ndiyo yalinigutusha kutoka usingizini. Mara nilisikia ile sauti nyororo kama kinanda ya ngoi ikiongoza wimbo, ambao kwa kawaida uliimbwa katika sherehe za arusi. Niligutuka kwa haraka, kuitupilia blanketi yangu mbali na kujisongeza dirishani na kupenyeza pazia. Kumbe kulikuwa kumekucha kwa kiasi hicho!

Shamshi lenye uhai lilikuwa lishachomoza, ishara kuwa ilikuwa mwanzo wa siku njema kwani siku njema huonekana asubuhi. Ingekuwa siku ya kukata na shoka kwani sahibu wangu Yohana angeuasi ukapera kwa kufunga akidi za maisha na kidosho Rebeka, waliyekutana na kupendana tangu tulipokuwa chuoni. Niliharakisha kujitayarisha ili nielekee kule kwani chelewachelewa utamkuta mwana si wako.

Takribani mwendo wa saa nne na nusu, mambo yalikuwa yametengenea. Kanisa lilikuwa limepambwa likapambika. Maputo ya kila aina na kila rangi yaliangikwa na kutundishwa ukutani. Tungu za mle kanisani zilimwayamwaya mwangaza na kufanya mle ndani kuwa mchana zaidi.Pengine kanisa lingekuwa likipambwa vile kila Jumapili, lingewavutia na kuwanata waumini chungu nzima. Mimbarini, mandishi makubwa ya rangi tofauti yalionekana na kusomeka eti: ‘REBEKA AOLEWA NA JOHANA ’

Mara ghafla Yohana na kundi lake liliwasili. Waume na vijana waliovalia nadhifu walimfuata unyounyo. Yohana alionekana mtanashati ajabu. Nilimhusudu. Ungelimwona msomaji wangu siku hiyo, usingelijua kuwa ndiye kijana aliyekuwa akipata adhabu siku zote shuleni kwa kuvalia sare zilizochakaa na kujaa makunyanzi kana kwamba zimetafunwa na ng’ombe na kisha kutemwa. Nywele zake daima zilisokotana kama vidude vya vinyesi vya mbuzi. Lakini kumbe maisha humbadili mtu. Pengine ni mapenzi ndiyo humafanya mja kubadilika.

Sasa Yohana alivalia suti nyeusi ti! na tai ndefu juu ya shati lake jeupe. Ndevu zake alizoziacha zilimwongezea haiba iliyofanya wengi kumtamani. Akapokelewa kwa shangwe kuu na kuingizwa kanisani.

Muda mfupi baadaye liliwasili kundi la bi arusi, Rebeka Mapesa na wafuasi wake.

Waliwashangaza mno waumini kwa namna walivyong’aa. Rebeka  mwenyewe alivalia nguo ndefu iliyomfunika hadi miguuni na kumpwayapwaya. Uso wake usingeuona kwani alikuwa kafunikwa kotekote. Sijui alionaje alikokuwa akikanyaga kwa kuwa mwendo wake ulikuwa wa mzofafa tena wa polepole kama kobe. Alikaribishwa na nyimbo za kuongoaongoa na kufuatilia zulia nyekundu waliyotandikiwa kuingia kanisani.

Kanisa lilijaa watu kutoka tabaka mbalimbali. Si wageni walioalikwa, si wazazi na watu wa jamii zote mbili na pia baadhi ya tuliosoma nao. Nyimbo ziliimbwa na masomo kutoka katika kitabu takatifu yakasomwa. Ikafika kilele. Wakati wa kuwaunganisha wawili hao. Kasisi aliyevalia mavazi meupe pe na nadhifu kana kwamba kukubaliana na ndoa yao alisonga mbele tayari kutenda kazi yake muhimu ya siku. Wawili wale wakawa wamesimama mbele yake. Kutoka nilikoketi, Rebeka alionekana malaika wa Mungu.

Wengi tulimmezea mate ndanindani lakini macho yake Yohana yalionekana kutuonya kuwa bahati ya mwenzio usiulalie mlango wazi. Aidha, nilikumbuka amri ya Mungu iliyoonya dhidi ya kutamani mali ya mtu mwingine.

“Kabla ya wawili hawa kuunganishwa na kufanywa kuwa kimoja, kuna yeyote aliye na pingamizi?” kimya kikuu kikaibia. Hakuna aliyejitokeza na swali likarudiwa mara mbili na kasisi. Kisha mwanaume mmoja aliyevalia nadhifu akanyanyuka kutoka kule alikoketi! Waumini nyoyo ziliwabapabapa na kuwaenda benibeni. Kila aliyeketi akawa ameachama, mdomo wazi kama pango la nyoka na kumtupia tazamo refu kama la mjusi. Mimi nilimjua kama Bohaz, kakake Yohana aliyesomea Ujerumani, akaishi na kufanya kazi huko. Alitaka tu kuhahikisha kuwa hakuna yeyote aliyepinga arusi ya nduguye. Ndio maana Yohana na mchumba wake hawakustushwa kamwe aliposimama. Lakini waumini hawakumjua ndio maana walishakata kauli mapema. Kumbe usilolijua ni kama usiku wa giza.

Ni wakati huo ndipo ilimjia msimamizi akilini kuwa pete zao zilisahaulika kule walikokuwa wakivalia na kufanyia mapambo ya Bi. Arusi. Alimnong’onezea kasisi mawili matatu na kuondoka kasi kama umeme. Kwa umbali kidogo, Yohana alionekana kukereketwa na kusinywa naye. Akatamani kumparamia na kumzabazaba makofi. Lakini alisimama patakatifu. Tena hakutaka kuonyesha hasira zake kwa umati. Pengine alikumbuka kuwa hasira hasara.

Wanakwaya wakaendelea kuwatumbuiza waumini na nyimbo za kikristo kwa furaha hata wakasahau kilichotokea. Wakadhihirisha bayana kuwa kuvunjika kwa mwiko sio mwisho wa mapishi. Waliendeleza nyimbo hadi msimamizi aliporejea muda si mrefu. Shughuli za awali zikaendelezwa. Maarusi wakakiri maneno baada ya kasisi na wakaanza kuvishana pete, huku kanisa zima limeja shangwe, vigelegele, hoihoi na nderemo pamoja na makofi ya furaha.

Kelele na furaha zilikatizwa ghafla na unyende kutoka nje. Mwanamke aliyeonekana chakaramu alikuwa akitimua mbio akielekea mimbarini. Alivaa nguo zilizoraruka na isitoshe alikuwa miguu mitupu.Maneno yalimtoka kwa sauti na haraka yasisikike vizuri. Vijitoto viwili vichafu vilimfuata pia mbiombio. Vilikuwa uchi na vilivyoparara ajabu! Mama yao alitamka kwa sauti kuwa Yohana alikuwa mumewe, baba ya vile vijototo. Eti walipendana na kuzaa vitoto hivyo kitambo kidogo Yohana alipokuwa angali chuoni! Kumbe ukistaajabu ya musa utayaona ya firauni.

Umati wa waumini uliduwaa na kuzuzuwaa. Kasisi bibilia ilimtoka mkononi na tang! Kuanguka sakafuni. Tayari vitoto vilianza kumpandiapandia Yohana na kumwitaita ‘baba.’ Yohana mwenyewe alipigwa na butwaa na akawa na mshtuko mkubwa. Parafujo za mwili wake ziliregea regerege na kukataa kumsimamisha imara. Rebeka alikuwa akifunzwa adabu na yule mwanamke chakaramu kwa kumwibia mume. Waumini wakajazana jukwani angalau kumwokoa. Nguo zake zilizokuwa nyeupe zilipata rangi mpya ya uwekundu. Mambo yalimwendea segemnenge na mvange, maji yakazidi unga na akazimia jukwani. Akawa amelala asijijue asijitambue. Jukwaa takatifu la Mungu likabadilishwa kuwa jukwaa la miereka na ndondi ya watu kupimana nguvu..

Naam, kilichoanza kwa mbwembwe na hanjam, sasa kilikuwa kikimalizika kwa fujo, rabsha, ghasia na vurumahi. Muumini mmoja alinivuta mabegani kwa nguvu akitaka kupita kuenda mbele kujionea sinema ya bure pia. Nikahisi uchungu wa ajabu na hapo ndipo niligituka na kupata kuwa misa ilikuwa imekwisha. Wanakwaya walikuwa wakiimba nyimbo za mwisho huku waumini wakiondoka na hapo ndipo mmoja alinigusa mbegani kuniamsha! Nilijinyanyua halahala kwa aibu hata sikutaka kuwatazama waumini walioonekana kunicheka. Kumbe nilikuwa nimelala muda huo wote kanisani mahubiri yalipokuwa yakiendelea na kupotelea katika ndoto hiyo! Niliapa kutoketi nyuma tena kila niingiapo kanisani kwa kuhofia kulala tena nyumbani mwa Bwana.

Hello world!

Standard

Welcome to WordPress.com. After you read this, you should delete and write your own post, with a new title above. Or hit Add New on the left (of the admin dashboard) to start a fresh post.

Here are some suggestions for your first post.

  1. You can find new ideas for what to blog about by reading the Daily Post.
  2. Add PressThis to your browser. It creates a new blog post for you about any interesting  page you read on the web.
  3. Make some changes to this page, and then hit preview on the right. You can always preview any post or edit it before you share it to the world.